MILIONI 123.3 ZAOKOLEWA, TAKUKURU YAIBUA MAPUNGUFU MNADA WA OLD SHINYANGA NA PAMBA KISHAPU | BUTONDO DIGITAL

Friday, November 13, 2026

MILIONI 123.3 ZAOKOLEWA, TAKUKURU YAIBUA MAPUNGUFU MNADA WA OLD SHINYANGA NA PAMBA KISHAPU

  Suzy Butondo       Friday, November 13, 2026


Na Suzy Butondo Shinyanga 

Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Shinyanga imefanikiwa kuokoa zaidi ya Shilingi milioni 123.3 kupitia ufuatiliaji wa ukusanyaji wa mapato kwa kutumia Mashine za Kielektroniki za POS katika Mnada wa Old Shinyanga pamoja na ufuatiliaji wa fedha za ununuzi wa zao la pamba katika Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu kwa msimu wa mwaka 2025/2026.

Akizungumza na waandishi wa habari  leo, Naibu Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Shinyanga, Mwamba Masanja, amesema mafanikio hayo yamepatikana katika kipindi cha kuanzia mwezi Aprili hadi Septemba 2026.

Masanja amesema kati ya fedha hizo, zaidi ya Shilingi milioni 75.5 zimeokolewa kupitia ufuatiliaji wa mapato katika Mnada wa Old Shinyanga uliopo Manispaa ya Shinyanga, ambapo ilibainika kuwa fedha zilizokusanywa hazikuwasilishwa benki kwa wakati kama inavyotakiwa

Amesema baada ya kufanya ufuatiliaji, TAKUKURU ilibaini baadhi ya mawakala waliokuwa wakikusanya ushuru kupitia mashine za POS walikuwa wakibakiza fedha hizo badala ya kuziwasilisha benki kwa mujibu wa taratibu.

"Baada ya ufuatiliaji huo, TAKUKURU ilibaini baadhi ya mawakala wa ukusanyaji ushuru kupitia POS walibaki na fedha hizo bila kuziwasilisha benki," amesema Masanja.


Aidha, Masanja amesema taasisi hiyo imefanikiwa kuokoa zaidi ya Shilingi milioni 47.7 zilizohusishwa na fedha za ununuzi wa zao la pamba katika msimu wa mwaka 2025/2026, kupitia ufuatiliaji uliofanyika katika Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu.

Amesema katika msimu huo, kampuni zilizopewa vibali vya kununua pamba zilikabidhi fedha kwa Vyama vya Msingi vya Ushirika wa Mazao (AMCOS) kwa ajili ya kununua pamba kutoka kwa wakulima.

Hata hivyo, amesema kupitia ufuatiliaji uliofanywa na TAKUKURU, hatua zilichukuliwa zilizosaidia kuhakikisha wakulima wanapata malipo yao.

Katika hatua nyingine, Masanja amesema TAKUKURU Mkoa wa Shinyanga inaendelea kutekeleza mikakati ya kuzuia rushwa katika robo ya pili ya mwaka kwa kuimarisha elimu kwa wananchi katika maeneo ya utoaji huduma pamoja na kufuatilia matumizi ya fedha za umma katika miradi mbalimbali ya maendeleo.

Amesisitiza kuwa juhudi hizo zinalenga kuhakikisha rasilimali za umma zinatumika kwa uwazi, uwajibikaji na kwa manufaa ya wananchi.

logoblog
Previous
« Prev Post