WANANCHI KISHAPU WAIOMBA SERIKALI KUKAMILISHA BARABARA YA KOLANDOTO MWANGONGO | BUTONDO DIGITAL

Tuesday, March 17, 2026

WANANCHI KISHAPU WAIOMBA SERIKALI KUKAMILISHA BARABARA YA KOLANDOTO MWANGONGO

  Suzy Butondo       Tuesday, March 17, 2026



Suzy Butondo,Shinyanga, Butondo Digital

 Baadhi ya wananchi wa wilaya ya  Kishapu Mkoani Shinyanga wameiomba Serikali kukamilisha ujenzi wa Barabara ya Kolandoto Mwangongo kwa kiwango cha lami  ili kurahisisha Shughuli za kimaendeleo wilayani hapo.


Wananchi  wameyasema hayo mbele ya Waziri  wa ujenzi Abdalah Ulega baada ya kukagua barabara hiyo, ambapo wamesema kwa sasa Shughuli zao za kiuchumi haziendi sawasawa kutokana na ubovu wa barabara inayounganisha wilaya ya kishapu na mkoa wa Simiyu

Elisha Elias mkazi wa  Kishapu na Idirisa Jabir wamesema  kwa sasa  hali ya barabara hiyo siyo rahisi kufanya shughuli zao za kimaendeleo, kwani wanashindwa kusafirisha vifaa mbalimbali kwa kuogopa vitaharibika.

"Kwanza tunashukuru kwa ujio wa waziri wa ujenzi, hivyo tunaamini barabara sasa litaanza kujengwa, tunaiomba sana serikali yetu itusaidie kwa hili ili na sisi tuweze kufanya shughuli mbalimbali za kiuchumi"amesema Jabir.

Kwa mujibu wa  meneja wa Wakala wa Barabara TANROADS mkoa wa Shinyanga Ntuli Mwaikokesya  amesema tayari zipo  hatua zilizoanza kuchukuliwa kwa ajili ya ujenzi wa barabara ambayo ni kilomita 52  
inayounganisha wilaya ya Kishapu na mkoa wa Simiyu.

Kwa upande wake Waziri wa ujenzi Abdalah Ulega baada ya kukagua balabala hiyo amesema tarehe 9,9,,2025 Rais Samia Suluhu Hassan alipita mji wa Maganzo wilaya ya Kishapu na kuahidi kwamba barabara hiyo ataifanikisha ili iweze kusaidia wananchi kiuchumi,  wakulima na wafanyabiashara mbalimbali.

"Kweli tunajua kwamba barabara hii ikikamilika itasaidia wafanyabiashara, wakulima, na kuleta maendeleo, hivyo naamini kama alivyoahidi Rais wetu kwamba ataitekeleza, kwani ni mkweli kuna ahadi nyingi tayari ameshazitekeleza na hii barabara ataitekeleza kwa awamu awamu.

"Hii kazi naomba mniachie mimi nitaibeba na nitahakikisha baada ya miaka mitatu minne itakuwa imeisha,hivyo kazi iliyobaki ni kuhakikisha tunapanga bajeti na kutoa kibali  cha kutangaza mkandarasi,kwani hii ni barabara muhimu sana kwa mkoa wetu"ameongeza Waziri Ulega.

Katika hatua nyingine waziri Ulega amekagua ujenzi wa uwanja wa ndege wa Mkoa wa  Shinyanga na kutoa maelekezo, kwamba kiwanja hicho kikamilishwe kwa wakati,  ikiwa ni pamoja na kuongezwa wafanyakazi na vitendea kazi ,  lakini pia Waziri amewapongeza viongozi wote wanaosimamia ujenzi huo na kuwaomba waendelee kusimamia ili kuhakikisha kinaanza kufanya kazi.

Waziri wa uchukuzi Abdalah Ulega akimsikiliza meneja wa TANROADS Mkoa wa Shinyanga

Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Julius Mtatiro akizungumza kwa niaba ya mkuu wa mkoa wa Shinyanga Mboni Mhita

Waziri wa uchukuzi Abdalah Ulega akimsikiliza meneja wa TANROADS Mkoa wa Shinyanga

Mwenyekiti wa chama cha mapinduzi CCM wilaya ya Shinyanga mjini Arnold Makombe akisalimiana na waziri wa uchukuzi Abdalah Ulega



logoblog
Previous
« Prev Post