MPIGA PICHA WA MKUU WA MKOA AFARIKI DUNIA, SABA WAJERUHIWA AJALI YA SAMUYE SHINYANGA | BUTONDO DIGITAL

Wednesday, May 20, 2026

MPIGA PICHA WA MKUU WA MKOA AFARIKI DUNIA, SABA WAJERUHIWA AJALI YA SAMUYE SHINYANGA

  Suzy Butondo       Wednesday, May 20, 2026

 

Mpiga picha wa mkuu wa mkoa Boaz Martine wakati wa uhai wake

Na Suzy Butondo, Shinyanga

Mtu mmoja amefariki dunia huku wengine saba wakijeruhiwa katika ajali ya barabarani iliyotokea Mei 20, 2026 katika kata ya Samuye, Halmashauri ya Shinyanga mkoani Shinyanga.

Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga, Janeth Magomi, amesema ajali hiyo ilihusisha gari aina ya Toyota Harrier lenye namba za usajili T 210 EDB na Toyota Land Cruiser Hardtop lenye namba DFPA 8920 mali ya shirika la KOICA, lililokuwa limebeba waandishi wa habari pamoja na watumishi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga.

Kwa mujibu wa Kamanda Magomi, marehemu ametambulika kuwa Boaz Martine, aliyekuwa mpiga picha wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga.

Majeruhi wa ajali hiyo ni Frank Mshana, Johnson James, Swahiba Msangi, pamoja na Neema Madono (36), Rehema Edson (45), Shadia Omari (32) na Laurence Piter (34). Wote wanaendelea kupatiwa matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga.

Kamanda Magomi amesema chanzo cha ajali hiyo ni uzembe wa dereva wa Toyota Harrier aliyekuwa akijaribu kulipita gari lililokuwa mbele yake bila kuchukua tahadhari, hali iliyosababisha kugongana na Land Cruiser hiyo kabla ya kuangukia mtaroni.

Aidha, ametoa wito kwa madereva kuzingatia sheria za usalama barabarani na kusisitiza kuwa Jeshi la Polisi litachukua hatua kali za kisheria dhidi ya madereva watakaobainika kusababisha ajali kwa uzembe, ikiwemo kufungiwa leseni na kufikishwa mahakamani.



logoblog
Previous
« Prev Post