
Suzy Butondo, Shinyanga – BUTONDO DIGITAL
Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Julius Mtatiro, amewataka wananchi wa Manispaa ya Shinyanga kuimarisha ushirikiano, kuishi kwa upendo na amani, pamoja na kujikita katika shughuli za maendeleo.
Ameyasema hayo kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mboni Mhita, wakati alipomwakilisha kwenye hafla ya Iftar iliyoandaliwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) mkoani Shinyanga.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mtatiro amesema Iftar hiyo ni sehemu muhimu ya kuimarisha mshikamano kati ya taasisi na jamii, ambapo Iftari hiyo imeandaliwa na TAKUKURU ili kuonesha upendo na kujenga ushirikiano na wananchi.
Amesisitiza kuwa rushwa ni adui wa haki na maendeleo, na kwamba wakati mwingine wananchi wenyewe pamoja na baadhi ya watumishi au waajiri huchangia kuwepo kwake.
Amewataka wananchi kutoa taarifa mapema wanapoona viashiria vya rushwa, akionya kuwa vitendo vya kupendelea au kupendelewa navyo ni rushwa vinavyopaswa kupigwa vita.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mhita, ameipongeza TAKUKURU kwa kuandaa Iftar hiyo, akisema inaonesha namna taasisi hiyo inavyowafikia wananchi na kudumisha ushirikiano mzuri na jamii.
Aidha, ameeleza kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, amefanya maendeleo makubwa mkoani Shinyanga, ikiwa ni pamoja na kukamilika kwa uwanja wa ndege, pamoja na kuongeza watumishi hasa katika sekta ya afya, wakiwemo madaktari bingwa.
Naye Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Shinyanga, Donnasian Kessy, amesema kuwa Iftar hiyo imeandaliwa katika mwezi mtukufu wa Ramadhani kwa Waislamu, pamoja na kipindi cha Kwaresma kwa Wakristo, ikiwa ni sehemu ya kuimarisha uhusiano na jamii.
Ameongeza kuwa mwitikio mkubwa wa wadau ni ishara njema kuwa jamii inaunga mkono juhudi za kupambana na rushwa, na akawasihi wananchi kuendelea kutoa taarifa wanapoona mianya ya rushwa ili hatua zichukuliwe kwa wakati.
Katika hatua nyingine, TAKUKURU imetoa msaada wa thamani ya zaidi ya shilingi 500,000 kwa Kituo cha Kulelea Watoto cha Kizumbi kilichopo Manispaa ya Shinyanga.

Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Julius Sunday Mtatiro,akizungumza na wananchi katika iftar ya jioni .

Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Shinyanga ,Donnasian Kessy akizungumza katika iftar ya jioni machi,18,2026



