Mhita ametoa agizo hilo wakati akifungua kikao cha Mkoa cha Kamati za Maafa kilichowakutanisha wakuu wa idara na taasisi za Serikali kutoka mkoani na wilayani, kwa ajili ya kuweka mikakati ya kukabiliana na athari zinazoweza kujitokeza wakati wa mvua za vuli zinazotarajiwa kuwa juu ya wastani.
Amesema maandalizi hayo ni muhimu kutokana na uwezekano wa mvua hizo kusababisha athari mbalimbali, ikiwemo mafuriko, hivyo amewataka viongozi na taasisi zinazohusika na masuala ya maafa kuhakikisha wanajiandaa mapema.
“Wakuu wa Wilaya wanapaswa kuhakikisha wanaongoza kamati za Maafa katika wilaya zao na kusimamia mipango pamoja na mikakati yote iliyowekwa ili kuzuia madhara yanayoweza kutokea,” amesema Mhita.
Aidha, Mkuu huyo wa Mkoa amesema timu ya Maafa ya Mkoa itakuwa na mawasiliano ya moja kwa moja na timu za maafa za wilaya, hatua ambayo itasaidia kurahisisha utoaji wa taarifa na uratibu wa hatua za haraka endapo kutatokea dharura.
Amesisitiza umuhimu wa kila idara na taasisi kutambua wajibu wake na kuhakikisha mipango ya kukabiliana na majanga inatekelezwa kwa wakati, ili kupunguza madhara kwa wananchi, mali na miundombinu.
