TABORA
Mbunge wa Jimbo la Tabora Mjini, Hawa Mwaifunga, amekutana na kufanya mazungumzo na Diwani wa Kata ya Chemchem, Bandora Salum Mirambo, kujadili changamoto zinazowakabili wakazi katika maeneo ya makazi na biashara yanayoathiriwa zaidi na mvua.
Mazungumzo hayo yamelenga kuweka mikakati madhubuti ya kukabiliana na athari zinazoweza kusababishwa na mvua za El Niño, pamoja na kuhakikisha changamoto zilizopo zinapatiwa ufumbuzi kwa wakati.
Katika mazungumzo hayo, Diwani Bandora ameeleza maeneo mbalimbali yenye changamoto, ikiwemo ukosefu wa kingo katika daraja la Mto Kenge, uhitaji wa makaravati, ubovu wa miundombinu katika baadhi ya mitaa, kuziba kwa mitaro kutokana na mchanga na taka, pamoja na maeneo ambayo hayana uelekeo mzuri wa maji wakati wa mvua.
Kufuatia changamoto hizo, Mbunge Hawa Mwaifunga ameahidi kutembelea Kata ya Chemchem Alhamisi, kwa lengo la kukagua maeneo hayo na kuweka mikakati ya pamoja itakayosaidia kuzuia au kupunguza athari za mvua.
Hatua hiyo inakuja kufuatia tahadhari iliyotolewa kuhusu uwezekano wa kuwepo kwa mvua kubwa, hali ambayo imeongeza umuhimu wa wananchi na viongozi kuchukua hatua za maandalizi mapema.
Aidha, Diwani Bandora amempongeza Mbunge Hawa Mwaifunga kwa jitihada zake za kusikiliza changamoto za wananchi na kuahidi kuyafikia maeneo yote yaliyoainishwa, akisisitiza umuhimu wa kushirikiana katika kutatua changamoto hizo.
Amesema hatua hizo zinaendana na msisitizo wa Serikali wa kuhakikisha changamoto zinazowakabili wananchi zinapatiwa ufumbuzi na huduma muhimu zinaimarishwa.
Aidha Bandora jana alikutana na wataalamu mbalimbali wa kata hiyo nakupanga leo ijumaa kuanza kufanya ziara ya kukagua maeneo mbalimbali zilizo na changamoto.

