Na Suzy Butondo, ShinyangaMkurugenzi wa Shule za Kom, Jackton Koyi, amewataka wahitimu wa Darasa la Saba na Chekechea kuendelea kudumisha nidhamu na upendo waliojengewa shuleni, wanaporejea katika familia na kwenye jamii zao.
Koyi ameyasema hayo hivi karibuni kwenye mahafali ya Shule ya Awali na Msingi Kom yaliyofanyika kwa ajili ya kuwaaga wahitimu wa Darasa la Saba na Chekechea.
Amesema shule hiyo itaendelea kushirikiana na wazazi kuhakikisha wanafunzi wanapata elimu bora, akiwashukuru wazazi kwa kuendelea kuwaamini na kuwapeleka watoto wao kusoma katika shule hiyo.
“Tunawashukuru wazazi kwa kutuamini na kutuletea watoto wenu katika shule yetu, hivyo niwaombe muendelee kutuamini kwa sababu hatutawaangusha bali tutaendelea kutoa huduma bora za elimu na kufanya vizuri kitaaluma,” amesema Koyi.
Aidha, amewataka wahitimu kuendelea kuwa na nidhamu na kuonyesha upendo wanapokuwa majumbani mwao.
Katika hatua nyingine Koyi ametangaza kuwa Septemba 22, 2026, kutakuwa na mtihani wa kujiunga na Kidato cha Kwanza katika Shule ya Sekondari Kom, huku fomu ya kujiunga ikigharimu Sh20,000 kwa kila mwanafunzi.
Amesema wanafunzi 83 waliohitimu Shule ya Awali na Msingi Kom tayari wamelipiwa fomu zao za kujiunga na shule hiyo.
Kwa upande wake, mgeni rasmi katika mahafali hayo, Afisa Mthibiti Ubora wa Shule katika Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga, Edith Mwijage, ambaye pia ni Mratibu wa Idara ya Uthibiti Ubora wa Shule Mkoa wa Shinyanga, amewapongeza wahitimu kwa kuonyesha nidhamu ya hali ya juu.
Mwijage amewataka wahitimu wanaporejea majumbani mwao kuendelea kuwa wanafunzi wenye nidhamu, huku akiwatahadharisha dhidi ya matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii, dawa za kulevya na kujiingiza katika makundi mabaya.
Amesema wahitimu hao wanakwenda kukutana na mazingira tofauti katika jamii, hivyo wanapaswa kuwa makini na kuendelea kutumia misingi mizuri waliyojengewa shuleni.
“Wanafunzi ambao mmehitimu Darasa la Saba, nendeni mkaitangaze Kom kwa kuendelea kuwa na nidhamu nzuri,” amesema Mwijage.
Aidha, ameipongeza Shule ya Awali na Msingi Kom kwa kuendelea kufanya vizuri kitaaluma na kufaulisha wanafunzi wake kwa kiwango cha daraja A.
Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Bodi ya Shule ya Awali na Msingi Kom, Beatrice Mark, amewataka wahitimu kuendelea kumtanguliza Mungu katika kila jambo, kujitambua na kusimamia ndoto zao.
Mark pia amewataka wazazi kuendelea kuwafuatilia na kuwasimamia watoto wao waliomaliza Darasa la Saba, akieleza kuwa dunia ya sasa ina changamoto mbalimbali, ikiwemo vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia.
Amesisitiza umuhimu wa wazazi kuwafundisha watoto namna ya kujilinda dhidi ya vitendo hivyo.
Akisoma taarifa ya shule, Mwalimu Mkuu wa Shule ya Awali na Msingi Kom, Pius Saye, amesema tangu kuanzishwa kwake, shule hiyo imeendelea kufanya vizuri kitaaluma kwa kupata ufaulu wa daraja A na B.
Kwa upande wa risala ya wanafunzi iliyosomwa na mhitimu Safina Nobert, amesema walipoanza shule walikuwa wanafunzi 56, lakini kutokana na mazingira mazuri ya kujifunzia na ufaulu mzuri wa shule hiyo, idadi iliongezeka hadi kufikia wanafunzi 83 ambao wamehitimu leo.