BANDORA AIPONGEZA KAMATI YA MAAFA, YAKAGUA MAENEO HATARISHI CHEMCHEM | BUTONDO DIGITAL

Thursday, November 12, 2026

BANDORA AIPONGEZA KAMATI YA MAAFA, YAKAGUA MAENEO HATARISHI CHEMCHEM

  Suzy Butondo       Thursday, November 12, 2026

 


Tabora

Diwani wa Kata ya Chemchem, Manispaa ya Tabora, Bandora Salum Mirambo, ameipongeza Kamati ya Maafa ya Halmashauri ya Manispaa ya Tabora, inayoongozwa na Mkurugenzi Dkt. John Pima, kwa kufanya ziara katika kata hiyo kwa lengo la kukagua maeneo hatarishi na kuweka mikakati ya kukabiliana na athari zinazoweza kusababishwa na mvua za El Niño.

Bandora ameipokea kamati hiyo na kushirikiana nayo katika kutembelea maeneo mbalimbali yanayotajwa kuwa hatarishi, yakiwemo maeneo ya Mto Kenge, ambao maji yake hutiririka kuelekea Shule ya Sekondari Kasongo, pamoja na makazi ya wananchi, ili kujionea hali halisi na kuchukua hatua za kuzuia madhara yanayoweza kujitokeza kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha.

Katika ziara hiyo, kamati ilikagua hali ya miundombinu, kubaini maeneo yenye changamoto na kutathmini utayari wa Kamati za Maafa za Kata katika kukabiliana na majanga yanayoweza kutokea.

Akizungumza baada ya ukaguzi huo, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Tabora, Dkt. John Pima, alitoa maelekezo kwa viongozi wa mitaa na kata kuendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu tahadhari za mvua, pamoja na kuhakikisha changamoto zinazojitokeza zinawasilishwa kwa wakati ili hatua za haraka ziweze kuchukuliwa.



Aidha, Dkt. Pima alishauri kuwekwa kwa vibao vya tahadhari katika maeneo hatarishi ili kuwaonya wananchi, kujengwa kwa kingo na madaraja ya dharura, pamoja na kuimarishwa kwa mikakati ya usalama katika maeneo yanayoweza kuathiriwa na mafuriko.

Pia aliwataka wananchi kuzingatia ushauri wa wataalamu na kufuata maelekezo yanayotolewa na viongozi, akisisitiza kuwa hatua hizo ni muhimu katika kulinda maisha ya watu, mali zao na mazingira dhidi ya athari za mvua.

logoblog
Previous
« Prev Post