BANDORA AZINDUA KIKUNDI CHA NZENGO CHEMCHEM, AHIMIZA UMOJA NA MSHIKAMANO | BUTONDO DIGITAL

Thursday, November 12, 2026

BANDORA AZINDUA KIKUNDI CHA NZENGO CHEMCHEM, AHIMIZA UMOJA NA MSHIKAMANO

  Suzy Butondo       Thursday, November 12, 2026

 


Tabora

Diwani wa Kata ya Chemchem, Manispaa ya Tabora, Bandora Salumu Mirambo, amefungua rasmi kikundi cha kijamii cha Nzengo katika Kata ya Chemchem, hafla iliyofanyika leo katika eneo la Barabara ya Tuwatugwe Mashineni.

Akizungumza katika hafla hiyo, Bandora amesema kuanzishwa kwa kikundi hicho ni hatua muhimu katika kuimarisha umoja, mshikamano na utamaduni wa kusaidiana miongoni mwa wananchi, hususan wakati wa misiba na kuwafariji wafiwa.

Aidha, Diwani huyo amewahimiza viongozi wa kikundi hicho kutekeleza majukumu yao kwa uwajibikaji, kusikiliza maoni ya wananchi na kuyafanyia kazi, huku akiwataka wananchi kushiriki kikamilifu katika vikao na kushirikiana na viongozi wa serikali za mitaa.

Katika hatua nyingine, Bandora amesisitiza umuhimu wa kudumisha maadili mema, kuheshimiana, kupendana na kuvumiliana katika jamii.

Amewataka wananchi kuepuka kuchanganya masuala ya dini, siasa, vyama na makabila katika shughuli za kijamii, akieleza kuwa mambo hayo yanaweza kusababisha migawanyiko na kudhoofisha umoja uliopo.

Vilevile, amewapongeza viongozi walioanzisha wazo la kuunda kikundi hicho, akisema ni mpango wenye manufaa makubwa katika kuwaunganisha wananchi na kujenga utamaduni wa kusaidiana wakati wa shida na furaha.

Hafla hiyo imehitimishwa na Diwani Bandora na kuongoza zoezi la harambee ya uchangiaji wa ufunguzi wa kikundi hicho ikiwa ni sehemu ya kuunga mkono juhudi za kuimarisha umoja na mshikamano katika Kata ya Chemchem.

logoblog
Previous
« Prev Post