Tabora
Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Dkt. Anjelina Mabula, amesema yuko tayari kushirikiana na kusapoti timu za mpira wa miguu zinazoshiriki Ligi ya Championship ili ziweze kufanya vizuri, kupanda daraja na hatimaye kushiriki Ligi Kuu ya Tanzania Bara.
Dkt. Mabula ameyasema hayo katika hafla ya makabidhiano ya ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Tabora kati yake na mtangulizi wake, baada ya kuwasili rasmi mkoani humo.
Akizungumzia kauli hiyo, Makamu Mwenyekiti wa Klabu ya Rhino Rangers, Bandora Salum Mirambo, amesema wamepokea kwa furaha kubwa ahadi hiyo ya Mkuu wa Mkoa, wakiamini kuwa itakuwa chachu ya mafanikio kwa timu za mkoa huo, hususan Rhino Rangers.
Bandora amesema uungwaji mkono kutoka kwa viongozi wa serikali ni muhimu katika kukuza michezo, kuinua vipaji na kuongeza morali kwa wachezaji pamoja na benchi la ufundi.
“Nimefurahishwa sana na kauli ya Mkuu wa Mkoa, Dkt. Anjelina Mabula, ya kuwa tayari kusapoti timu zetu. Ni jambo la kufurahisha kuona viongozi wakionesha utayari wa kuunga mkono michezo. Uungwaji mkono huo utasaidia kukuza vipaji, kuongeza hamasa na ari kwa wachezaji,” amesema Bandora.
Ameongeza kuwa wanaamini ushirikiano kati ya viongozi wa serikali na wadau wa michezo utasaidia kuimarisha soka la Mkoa wa Tabora na kufungua fursa zaidi kwa timu zake kufanya vizuri katika mashindano mbalimbali.

