
Suzy Butondo
SHINYANGA – Waziri wa Nishati, Deogratius Ndejembi, amesaini mkataba wa utekelezaji wa awamu ya pili ya mradi wa kuzalisha umeme wa jua wenye uwezo wa megawati 100 utakaogharimu zaidi ya Shilingi bilioni 204, huku akisisitiza ajira kwa wananchi wa eneo husika na ujenzi wa vyumba vitano vya madarasa kupitia mpango wa uwajibikaji kwa jamii (CSR).
Mkataba huo ulisainiwa kati ya Tanesco na mkandarasi Sagemcom GIS kwa ufadhili wa Shirika la Maendeleo la Ufaransa (AFD). Mradi huo utatekelezwa katika Kijiji cha Ngunga, wilayani Kishapu mkoani Shinyanga, kwa kipindi cha miezi 17, huku muda wa matazamio ya kukamilika ukiwa miezi 24.
Akizungumza katika hafla ya utiaji saini wa mkataba huo, Waziri Ndejembi alisema mradi huo ni mwendelezo wa awamu ya kwanza iliyosainiwa mwaka 2021 chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan.
Alisema awamu ya kwanza ilizalisha megawati 50 ambazo tayari zimeunganishwa kwenye Gridi ya Taifa, huku awamu ya pili ikiongeza megawati 100 na kufanya jumla ya uzalishaji wa umeme wa jua katika eneo hilo kufikia megawati 150.
"Awamu ya kwanza iligharimu Shilingi bilioni 118 kwa uzalishaji wa megawati 50. Awamu ya pili itatumia zaidi ya Shilingi bilioni 204 kuzalisha megawati 100, hivyo kufanya jumla ya uwekezaji kufikia zaidi ya Shilingi bilioni 320," alisema Ndejembi.
Aliielekeza Tanesco kuhakikisha mradi huo unakamilika kwa wakati na kuendelea kutekeleza miradi ya maendeleo kwa wananchi ikiwemo ujenzi wa vyumba vitano vya madarasa, kusambaza umeme katika maeneo yaliyobaki na kupeleka huduma hiyo kwenye taasisi za umma.
Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco, Lazaro Twange, alisema awamu ya kwanza ya mradi imefikia asilimia 96.7 ya utekelezaji na megawati 50 tayari zimeunganishwa kwenye Gridi ya Taifa.
Alisema mwaka 2023 Tanesco ilisaini mkataba na Shirika la Maendeleo la Ufaransa (AFD), ambalo lilitoa euro milioni 43 kufadhili awamu ya kwanza iliyotekelezwa kwa kushirikiana na kampuni ya Sinohydro ya China kwa gharama ya Shilingi bilioni 118.
Twange alisema mradi huo umekuwa na manufaa makubwa kwa wananchi wa Ngunga, ikiwemo kujengwa kwa madarasa mawili, ugawaji wa miche ya miti, mizinga 60 ya nyuki, pamoja na kuwapatia wakazi pembejeo za kilimo na huduma za kulima mashamba.
Kwa mujibu wa Twange, awamu ya pili inafadhiliwa na Serikali ya Ufaransa kupitia AFD kwa euro milioni 76 na itahusisha ujenzi wa kituo cha megawati 100, zahanati, miradi ya maji na kukamilisha usambazaji wa umeme katika kitongoji pekee ambacho bado hakijafikiwa na huduma hiyo.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati anayeshughulikia Umeme na Nishati Jadidifu, Mhandisi Felchesmi Mramba, alisema umeme wa jua ni miongoni mwa vyanzo vinavyokua kwa kasi duniani kutokana na gharama zake kuwa nafuu na mchango wake mkubwa katika uzalishaji wa nishati.
Alisema Tanzania itaendelea kuwekeza katika nishati jadidifu ili kuongeza upatikanaji wa umeme na kuimarisha maendeleo ya kiuchumi.
Mbunge wa Kishapu, Lucy Mayenga, aliushukuru Serikali kwa kupeleka mradi huo katika jimbo lake na kuomba vijana wa eneo hilo wapewe kipaumbele cha ajira wakati wa utekelezaji wa mradi pamoja na kuendelea kujengwa kwa miundombinu ya elimu.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mboni Mhita, alisema uwekezaji wa zaidi ya Shilingi bilioni 320 katika awamu zote mbili za mradi huo ni historia kwa mkoa huo, akisisitiza kuwa wananchi wataendelea kuulinda na kuutunza ili ulete manufaa ya kudumu.




