TAIFA GROUP YATANGAZA KUREJEA KWA SHUGHULI ZA NATION MEDIA GROUP NCHINI UGANDA | BUTONDO DIGITAL

Tuesday, July 28, 2026

TAIFA GROUP YATANGAZA KUREJEA KWA SHUGHULI ZA NATION MEDIA GROUP NCHINI UGANDA

  Suzy Butondo       Tuesday, July 28, 2026

 Kampuni ya Taifa Group imetangaza kurejea kwa shughuli za kampuni yake tanzu ya Nation Media Group nchini Uganda kufuatia idhini iliyotolewa na Rais wa Uganda, Yoweri Kaguta Museveni.

Uamuzi huo unatajwa kuwa hatua muhimu katika kuimarisha uwekezaji wa kikanda, maendeleo ya sekta ya habari na ushirikiano wa kiuchumi ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Kupitia kampuni yake tanzu ya Taarifa Limited, Taifa Group ndiyo mbia mkuu wa Nation Media Group na inaendelea kujizatiti katika kuendeleza uwekezaji wenye uwajibikaji, utawala bora wa kampuni na maendeleo endelevu katika ukanda wa Afrika Mashariki.

Akizungumzia hatua hiyo, Mwenyekiti wa Taifa Group, Bw. Rostam Azizi, alimshukuru Rais Yoweri Kaguta Museveni kwa kuruhusu kurejea kwa shughuli za Nation Media Group nchini Uganda.

Pia alimshukuru Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi ya Uganda (UPDF), Jenerali Muhoozi Kainerugaba, kwa mchango wake katika kufanikisha mchakato huo.

"Ningependa kutoa shukrani zangu za dhati kwa Mheshimiwa Rais Yoweri Kaguta Museveni kwa uamuzi huu muhimu, na kwa Jenerali Muhoozi Kainerugaba kwa uungaji mkono wake katika mchakato mzima uliopelekea matokeo haya chanya."

Alisema Taifa Group inaendelea kuwa na dhamira ya kuchangia maendeleo ya kijamii na kiuchumi ya Uganda kupitia uwekezaji wenye uwajibikaji, ushirikiano wa muda mrefu na ujenzi wa thamani endelevu.

"Kama mbia mkuu wa Nation Media Group, tunaunga mkono kikamilifu dhamira ya kampuni hiyo ya kuzingatia misingi ya uandishi wa habari wa haki, uwiano, uhuru na uwajibikaji. Tunaamini vyombo vya habari imara na vya kitaalamu vina nafasi muhimu katika kuimarisha maendeleo ya taifa, utawala bora na ushirikiano wa kikanda."

Aidha, alisema uamuzi huo unaonyesha umuhimu wa mazungumzo, kuheshimiana na ushirikiano wa kikanda.
"Taifa Group itaendelea kuwekeza katika fursa zinazozalisha ajira, kuimarisha taasisi na kuchochea ustawi wa pamoja katika Afrika Mashariki."

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Nation Media Group, Bw. Joe Muganda, alisema kampuni hiyo sasa itaelekeza nguvu zake katika kujenga upya uwepo wake nchini Uganda na kuimarisha huduma zake kwa wasomaji, watazamaji na wadau wengine.

"Tunakaribisha fursa ya kurejesha shughuli nchini Uganda na kuunganishwa tena na watazamaji wetu, wafanyakazi, washirika wa kibiashara na jamii. Kipaumbele chetu kitakuwa kurejesha majukwaa yetu kwa uwajibikaji, kuimarisha maudhui ya ndani na kuwapa Waganda uandishi wa habari wa kuaminika, muhimu na wa ubunifu kupitia magazeti, matangazo na majukwaa ya kidijitali."

Aliongeza kuwa Nation Media Group itatumia uzoefu wake wa kikanda kusaidia ukuaji wa tasnia ya habari nchini Uganda huku ikifungua fursa zaidi kwa vipaji, biashara na ushiriki wa umma.

Kurejea kwa shughuli za Nation Media Group nchini Uganda kunaakisi uhusiano imara kati ya Tanzania na Uganda pamoja na dhamira ya serikali za Afrika Mashariki na sekta binafsi ya kuimarisha utangamano wa kikanda, uwekezaji wa mipakani na ushirikiano wa kiuchumi.

Kadiri Nation Media Group inavyojenga upya shughuli zake nchini Uganda, itaendelea kutumia uwepo wake nchini Kenya, Uganda, Tanzania na Rwanda kuunganisha watazamaji, kuimarisha mazungumzo ya kikanda na kuchangia maendeleo ya kijamii na kiuchumi ya Afrika Mashariki.

Taifa Group imesisitiza kuwa itaendelea kushirikiana na serikali, taasisi, wafanyabiashara na jamii katika ukanda mzima ili kupanua fursa za kiuchumi endelevu na kuimarisha ustawi wa muda mrefu wa Afrika Mashariki.
































logoblog
Previous
« Prev Post