WATUMISHI WA MANISPAA YA SHINYANGA WATAKIWA KUWAFUATA WANANCHI: KERO ZA MIKOPO NA MASOKO ZATAJWA | BUTONDO DIGITAL

Thursday, July 30, 2026

WATUMISHI WA MANISPAA YA SHINYANGA WATAKIWA KUWAFUATA WANANCHI: KERO ZA MIKOPO NA MASOKO ZATAJWA

  Suzy Butondo       Thursday, July 30, 2026

 



Suzy Butondo, Shinyanga

Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake wa Chama Cha Mapinduzi (UWT) Wilaya ya Shinyanga Mjini, Rehema Nhamanilo, amewataka watumishi wa Serikali katika Manispaa ya Shinyanga kutoka maofisini na kuwafuata wananchi ili  kusikiliza na kutatua changamoto zinazowakabili badala ya kusubiri wananchi wafike ofisini.

Nhamanilo ametoa kauli hiyo wakati wa ziara ya Kamati ya Utekelezaji ya UWT Wilaya ya Shinyanga Mjini ya kukutana na wanawake katika kata 17 za manispaa hiyo kwa lengo la kuimalisha chama, kusikiliza kero zao na kujadili fursa za maendeleo.

Katika mikutano hiyo, wanawake walieleza kuwa wanakabiliwa na changamoto mbalimbali, ikiwemo ugumu wa kupata mikopo ya halmashauri kutokana na ukosefu wa elimu, usimamizi hafifu wa watendaji na kushindwa kufikiwa na taarifa muhimu kuhusu fursa zilizopo.

"Watendaji wote wajitathmini, haiwezekani baadhi ya kata zikose wanufaika wa mikopo kwa sababu ya uzembe wa watendaji. Wanapaswa kuwafuata wananchi na kuwapa elimu kuhusu fursa zilizopo," alisema Nhamanilo.

Aliwataka pia viongozi wa kata na matawi kushuka kwa wananchi mara kwa mara ili kusikiliza changamoto zao na kushirikiana katika kuzitafutia ufumbuzi.

Aidha, aliwahimiza wanawake kujiunga katika vikundi vya kiuchumi ili waweze kunufaika na mikopo inayotolewa kupitia halmashauri, Ofisi ya Waziri Mkuu pamoja na taasisi za kifedha kama CRDB na NMB, badala ya kukimbilia mikopo yenye riba kubwa inayojulikana kama mikopo umiza.

Mbali na mikopo, wanawake walieleza kero nyingine zinazowakabili, zikiwemo msongamano katika Soko la Nguzo Nane, ukosefu wa maeneo rasmi ya kufanyia biashara, ucheleweshaji wa huduma ya ukusanyaji taka, pamoja na ukosefu wa Afisa Afya katika eneo la Shinyanga Mjini.

Walisema changamoto hizo zimekuwa zikiathiri shughuli zao za kila siku na kuwakwamisha kujiongezea kipato.

Akijibu baadhi ya hoja hizo, Meya wa Manispaa ya Shinyanga, Salum Kitumbo, alisema halmashauri inaendelea na maboresho ya soko kuu ili kupunguza msongamano na kuboresha mazingira ya wafanyabiashara.

Alisema pia hatua zimeanza kuchukuliwa kudhibiti malori makubwa yanayoingia katikati ya mji, huku akiahidi kusimamia kwa karibu utoaji wa mikopo ili kuhakikisha walengwa halali wanapata fursa hiyo.

"Nitasimamia mwenyewe kuhakikisha wanawake wanaostahili wanapata mikopo,nawahimiza kuunda vikundi na kutumia mikopo hiyo kwa shughuli za maendeleo ili waweze kujikwamua kiuchumi," alisema Kitumbo.

Hata hivyo leo mwenyekiti wa UWT Wilaya ya Shinyanga Mjini Rehema Nhamanilo akiwa na viongozi wake wa kamati ya utekelezaji amehitimisha kwa kishindo ziara yake katika kata ya Ibinzamata, ambapo ametembelea kata 17 za manispaa, ambayo ilikuwa na lengo la kuimalisha uhai wa chama, kusikiliza kero za wananchi, kuhamasisha ushiriki wa wanawake katika shughuli za maendeleo na kuhakikisha huduma za Serikali zinawafikia wananchi kwa ufanisi.

Angalia Picha za matukio mbalimbali👇
Mwenyekiti wa UWT wilaya ya Shinyanga mjini Rehema Nhamanilo akizungumza na wanawake wa kata ya Ndala


Mwenyekiti wa UWT wilaya ya Shinyanga mjini Rehema Nhamanilo akizungumza na wanawake wa kata ya mjini
Diwani viti maalumu manispaa ya Shinyanga mjini Veronica Masawe akiwa amepiga Magoti akiwashukuru kwa kushiriki vizuri kwenye uchaguzi mkuu
Diwani viti maalumu manispaa ya Shinyanga mjini Mwanahamis Kazoba akizunguma
Diwani viti maalumu manispaa ya Shinyanga mjini Mwanaid akizungumza
Diwani viti maalumu manispaa ya Shinyanga mjini Veronica Masawe akizungumza
Naibu Meya wa manispaa ya Shinyanga Pendo Sawa akiwa amepiga magoti akiwashukuru wanawake kwa kushiriki vizuri kwenye uchaguzi
Naibu Meya wa manispaa ya Shinyanga Pendo Sawa akizungumza
Diwani wa kata ya Ndala Zamda Shaban akifafanua jambo

Mwenyekiti wa UWT wilaya ya Shinyanga mjini Rehema Nhamanilo akizungumza na wanawake wa kata ya Kitangili
Mjumbe wa halmashauri kuu ya wilaya ya Shinyanga mjini Rabia Ally akizungumza

Diwani wa kata ya Ngokolo Jackline Isalo akizungumza baada ya kamati ya utekelezaji ya ya UWT wilaya kutembelea katika kata hiyo




Mjumbe wa kamati ya utekelezaji Juliana Buzuruga akizungumza kwenye mkutano huo






Katibu wa UWT kata ya Ndembezi Christina akitambulisha viongozi wa UWT kata ya Ndembezi baada ya kamati ya utekelezaji kutembelea Kata Hiyo
Mjumbe Wa kamati ya utekelezaji Mariam Kajala akizungumza kwenye mkutano huo


Meya Wa manispaa ya Salum Kitumbo akizungumza kwenye mkutano wa UWT


























 




















































logoblog
Previous
« Prev Post