BANDORA AWATAKA VIONGOZI NA WATAALAMU KUONGEZA KASI YA MAENDELEO | BUTONDO DIGITAL

Friday, July 31, 2026

BANDORA AWATAKA VIONGOZI NA WATAALAMU KUONGEZA KASI YA MAENDELEO

  Suzy Butondo       Friday, July 31, 2026









CHEMCHEM  – Mwenyekiti wa Kamati ya Maendeleo ya Kata (WDC) ya Chemchem na Diwani wa Kata hiyo, Bandora Salum Mirambo, ameweka wazi msimamo wake wa kuharakisha maendeleo ya kata hiyo kwa kusisitiza uwajibikaji, ushirikiano na utekelezaji wa mipango madhubuti kutoka kwa viongozi na wataalamu.

Akiongoza kikao cha Kamati ya Maendeleo ya Kata kilichowakutanisha wataalamu wa kata pamoja na wenyeviti wa mitaa, Bandora alisema mafanikio ya Chemchem yatapatikana endapo kila mmoja atatimiza wajibu wake kwa ufanisi na kuweka maslahi ya wananchi mbele.

Alieleza kuwa kuna umuhimu wa kuimarisha mipango ya maendeleo inayolenga kuongeza tija katika utoaji wa huduma, huku akitaka juhudi zaidi zielekezwe kwenye ukusanyaji wa mapato ya ndani ili kuongeza uwezo wa kutekeleza miradi ya maendeleo.

Mbali na hilo, Bandora alisisitiza kuimarishwa kwa ulinzi na usalama ili wananchi waendelee kufanya shughuli zao za kijamii na kiuchumi katika mazingira ya amani na utulivu.

Kwa upande wa viongozi wa mitaa, aliwataka kufanya mikutano ya mara kwa mara na wananchi ili kusikiliza kero zao na kuzitafutia ufumbuzi kwa wakati. Aidha, aliwakumbusha wataalamu wa kata kutekeleza majukumu yao kwa weledi, uadilifu na kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za kazi.

Bandora alisema uwajibikaji wa kila kiongozi na mtumishi wa umma ni nguzo muhimu ya kufanikisha agenda ya maendeleo ya Kata ya Chemchem, sambamba na kuunga mkono jitihada za Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan.

"Kazi na Utu, Tunasonga Mbele" ndiyo kaulimbiu inayozidi kuhamasisha utekelezaji wa majukumu kwa bidii na mshikamano katika kuijenga Chemchem yenye maendeleo endelevu.

logoblog
Previous
« Prev Post