
Siku ya Gawio si siku ya kusherehekea mafanikio ya kifedha pekee, bali pia ni fursa ya kufanya tathmini ya kina kuhusu maeneo yanayohitaji maboresho zaidi ili kuhakikisha mafanikio haya yanakuwa endelevu na yanazidi kuimarika mwaka hadi mwaka.
Mafanikio haya yanathibitisha kuwa taasisi na mashirika ya umma yana uwezo wa kutoa huduma bora kwa wananchi huku yakichangia kikamilifu katika ujenzi wa uchumi imara wa taifa.
Tunapojiandaa kuanza utekelezaji wa Dira ya Taifa 2050, ni muhimu kutambua kuwa hatutaweza kujenga uchumi wenye ushindani kwa kutegemea taasisi zinazofanya kazi kwa mazoea. Ni lazima tujenge utamaduni wa uwajibikaji unaopima mafanikio kwa matokeo halisi na athari chanya kwa wananchi, badala ya kutegemea takwimu pekee. Huo ndio mwelekeo na maono ya taifa letu.
Ninazipongeza taasisi na mashirika yote yaliyotoa gawio kwa mchango wao katika kuongeza mapato ya ndani ya Serikali, ambayo ni nguzo muhimu ya kugharamia miradi na shughuli za maendeleo. Hata hivyo, pongezi hizi zisiwe sababu ya kuridhika au kubweteka.
Serikali itaendelea kusimamia kwa karibu utendaji wa taasisi zote na haitasita kuchukua hatua stahiki pale itakapobaini uzembe, matumizi mabaya ya rasilimali za umma au ukiukwaji wa misingi ya uwajibikaji.