SHINYANGA YAZINDUA KITUO CHA UTALII IKOLOJIA LUBAGA, KUFUNGUA FURSA MPYA ZA AJIRA NA UHIFADHI | BUTONDO DIGITAL

Monday, June 29, 2026

SHINYANGA YAZINDUA KITUO CHA UTALII IKOLOJIA LUBAGA, KUFUNGUA FURSA MPYA ZA AJIRA NA UHIFADHI

  Suzy Butondo       Monday, June 29, 2026


 Na Suzy Butondo, Shinyanga 

Mkoa wa Shinyanga umeandika ukurasa mpya katika maendeleo ya sekta ya utalii baada ya kuzinduliwa rasmi Kituo cha Utalii Ikolojia (Ecotourism Centre) ndani ya Msitu wa Hifadhi wa Lubaga, hatua inayolenga kuifanya hifadhi hiyo kuwa moja ya vivutio vikubwa vya utalii wa mazingira nchini huku ikichochea uchumi wa wananchi na kuimarisha juhudi za uhifadhi wa misitu.

Uzinduzi huo umefanyika katika Msitu wa Hifadhi wa Lubaga uliopo Manispaa ya Shinyanga, ambapo Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Frank Nkinda, alimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga. Hafla hiyo iliwakutanisha viongozi wa Serikali, Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), wadau wa uhifadhi, sekta ya utalii pamoja na wananchi.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Nkinda amesema mradi huo unaashiria mwelekeo mpya wa kutumia rasilimali za asili kama chachu ya maendeleo ya kiuchumi bila kuathiri mazingira.

Amesema kwa miaka mingi wengi wamekuwa wakitazama utalii kupitia mbuga za wanyama, milima na fukwe za bahari, lakini Msitu wa Hifadhi wa Lubaga umeonyesha kuwa hata misitu inaweza kuwa kivutio kikubwa cha utalii kinachozalisha ajira, mapato na kutoa elimu kuhusu uhifadhi wa mazingira.

"Shinyanga ina utajiri mkubwa wa maliasili unaoweza kutumika kuinua uchumi wa wananchi. Tunataka wananchi waone kuwa utalii haupo mbali; unaanzia hapa hapa walipo," amesema Nkinda.

Ameeleza kuwa maendeleo ya utalii wa ndani yataongeza mapato ya Serikali, kupanua fursa za biashara kwa wananchi, kuhamasisha uhifadhi wa mazingira na kukuza utamaduni wa kuthamini urithi wa asili.

Aidha, ametoa wito kwa wananchi, shule, vyuo, taasisi na makampuni kutumia kituo hicho kwa shughuli za mafunzo, tafiti, mapumziko na burudani, akibainisha kuwa maeneo ya asili yana mchango mkubwa katika kuboresha afya ya mwili na akili.

Pia amewahimiza vijana kutumia fursa zinazotokana na utalii wa mazingira kujiajiri kupitia huduma za utalii, biashara ndogo ndogo, ufugaji wa nyuki na shughuli nyingine zinazohusiana na uhifadhi wa mazingira.

Kwa upande wake, Mhifadhi Mwandamizi wa Misitu wa TFS Wilaya ya Shinyanga, Fabian Balele, amesema ujenzi wa kituo hicho umefanyika kwa kuzingatia misingi ya uhifadhi, ambapo hakuna mti hata mmoja uliokatwa wakati wa utekelezaji wa mradi huo.

Amefafanua kuwa miundombinu yote imejengwa katika maeneo ambayo hayaharibu mfumo wa ikolojia wa msitu, ikiwa ni sehemu ya kuhakikisha maendeleo yanaenda sambamba na uhifadhi wa mazingira.

Kwa sasa kituo hicho kinatoa huduma mbalimbali za utalii ikiwemo matembezi ya misituni, utalii wa baiskeli, maeneo maalumu ya kupiga picha, ukumbi wa mikutano, maeneo ya kupiga kambi (Camping Sites), picnic pamoja na Special Moments Corner, eneo maalumu kwa shughuli za kijamii kama uchumba na matukio mengine.

Mbali na huduma hizo, wageni wanaotembelea Lubaga watapata fursa ya kujifunza kuhusu ufugaji wa nyuki kupitia Apitourism, pamoja na elimu ya utunzaji wa miti, mimea tiba na uhifadhi wa mazingira.

Balele amesema TFS inaendelea kuboresha kituo hicho kwa kuongeza vivutio vipya vitakavyokifanya kuwa kitovu cha utalii wa mazingira katika Kanda ya Ziwa.

Miongoni mwa miradi iliyopangwa ni ujenzi wa mabwawa ya kuogelea, bustani ya wanyama, viwanja vya michezo mbalimbali, ukumbi mkubwa wa mikutano na matukio, ukumbi wa mazoezi (Gym) pamoja na sehemu za michezo kwa watoto.

Naye Mwakilishi wa Kamanda wa TFS Kanda ya Magharibi, Aloyce Kilemwa, amesema mradi huo ni sehemu ya mkakati wa kuongeza thamani ya misitu ya hifadhi kupitia utalii endelevu unaolinda mazingira huku ukizalisha manufaa ya kiuchumi kwa Serikali na wananchi.

Kwa upande wake, Mwakilishi wa Meya wa Manispaa ya Shinyanga na Diwani wa Kata ya Ngokolo, Jackline Isaro, amesema uzinduzi wa Kituo cha Utalii Ikolojia cha Lubaga unaunga mkono juhudi za Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan za kuitangaza Tanzania kupitia kampeni ya Royal Tour, ambayo imeongeza utambulisho wa vivutio vya utalii vya nchi kimataifa.

Amesema Manispaa itaendelea kushirikiana na TFS kutangaza kivutio hicho ili kuongeza idadi ya watalii na kuhakikisha wananchi wanapata manufaa ya moja kwa moja kupitia ukuaji wa sekta ya utalii.

Kuzinduliwa kwa Kituo cha Utalii Ikolojia cha Lubaga kunatajwa kuwa hatua muhimu katika kuifanya Shinyanga kuwa miongoni mwa maeneo yanayoongoza kwa utalii wa mazingira nchini, huku kikifungua fursa mpya za uwekezaji, ajira, biashara na kuimarisha uhifadhi wa misitu kwa manufaa ya vizazi vya sasa na vijavyo.
Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Frank Nkinda, akimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mboni Mhita
Mwakilishi
wa Kamanda wa Kanda TFS Aloyce Nkilemwa akizungumza.
Afisa Mwandamizi wa uhifadhi wa Misitu kutoka TFS Wilaya ya Shinyanga Fabian Balele akizungumza.












logoblog
Previous
« Prev Post