*HAIUZWI!” KITENDAWILI CHA RC MABULA CHATEGULIWA, RHINO RANGERS YAPIGIWA MSTARI | BUTONDO DIGITAL

Tuesday, November 17, 2026

*HAIUZWI!” KITENDAWILI CHA RC MABULA CHATEGULIWA, RHINO RANGERS YAPIGIWA MSTARI

  Suzy Butondo       Tuesday, November 17, 2026

 


Tabora

Kilianza kama kitendawili! Kauli ya maneno mawili, “HAIUZWI”, iliibua maswali mengi miongoni mwa wananchi. HAIUZWI nini? Kwa nini haiuzwi? Ni kitu gani kilichokuwa nyuma ya kauli hiyo?

Kauli hiyo ilitolewa na Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Dkt. Anjelina Mabula, Novemba 9, 2026, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari. Hata hivyo, kauli yake ya “HAIUZWI, na haya ni maelekezo” iliendelea kuwaacha wananchi katika mshangao na maswali mengi kuhusu alichokuwa akimaanisha.

Hatimaye, Novemba 13, 2026, kitendawili hicho kiliteguliwa! Ikafahamika kuwa kilichokuwa hakipaswi kuuzwa ni timu ya Rhino Rangers, inayobeba fahari na matumaini ya mashabiki wa soka wa Mkoa wa Tabora.

Kauli hiyo iliambatana na hafla ya harambee ya kuchangia timu ya Rhino Rangers, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuimarisha timu hiyo kupitia ushiriki na michango ya wananchi pamoja na wadau mbalimbali wa soka.

Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Dkt. Anjelina Mabula, ameonesha wazi kuwa ni miongoni mwa viongozi wanaopenda maendeleo ya michezo, hususan soka. 

Tangu alipokabidhiwa rasmi ofisi ya Mkuu wa Mkoa, alieleza utayari wake wa kuiunga mkono Rhino Rangers na kuhakikisha inapata nguvu ya kufanya vizuri ili kufikia ndoto ya kupanda kucheza Ligi Kuu Tanzania Bara msimu ujao.

Jitihada za kuhamasisha maendeleo ya soka mkoani Tabora pia ziliibuliwa Novemba 3, 2026, na Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Tabora, Said Nkumba, aliyemtaka Mkuu wa Mkoa kuhakikisha timu zinazoshiriki mashindano mbalimbali zinapata ushirikiano na sapoti inayostahili.

Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa Rhino Rangers, Bandora Salum Mirambo, amepongeza jitihada zinazofanywa na Mkuu wa Mkoa pamoja na wadau wengine katika kuimarisha timu hiyo.

Aidha, amewataka wananchi na wadau wa michezo kujitokeza kwa wingi kuisapoti Rhino Rangers kwa hali na mali, akieleza kuwa ushiriki wao ni muhimu katika kuijenga timu na kuifikisha kwenye malengo yake.

Sasa ujumbe umeeleweka, kitendawili kimepata jibu na msimamo umewekwa wazi.

RHINO RANGERS HAIUZWI!

Fahari ya Tabora, jukumu la wanatabora wote!

logoblog
Newest
You are reading the newest post