BANDORA AKUTANA NA DAS ASHA CHURU, WAWEKA MIKAKATI YA KULETA MAENDELEO CHEMCHEM | BUTONDO DIGITAL

Tuesday, November 3, 2026

BANDORA AKUTANA NA DAS ASHA CHURU, WAWEKA MIKAKATI YA KULETA MAENDELEO CHEMCHEM

  Suzy Butondo       Tuesday, November 3, 2026

 


Tabora
Diwani wa Kata ya Chemchem katika Manispaa ya Tabora, Bandora Salum Mirambo, amekutana na kufanya mazungumzo na Katibu Tawala wa Wilaya ya Tabora (DAS), Asha Churu, katika ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Tabora, kwa lengo la kuimarisha ushirikiano na kuweka mikakati ya kuharakisha maendeleo.

Mazungumzo hayo yamelenga kuimarisha mahusiano na ushirikiano kati ya Ofisi ya Katibu Tawala wa Wilaya na Ofisi ya Diwani wa Kata ya Chemchem, ili kuongeza ufanisi na weledi katika utekelezaji wa majukumu ya kuwahudumia wananchi.

Akizungumzia mazungumzo hayo, Diwani Bandora amesema wamekubaliana kuweka mikakati ya kubuni na kuanzisha miradi mbalimbali ya maendeleo itakayowapatia wananchi fursa za kiuchumi, kuongeza mapato na kuleta tija kwa Kata ya Chemchem pamoja na Wilaya ya Tabora kwa ujumla.

Amesisitiza kuwa lengo la mikakati hiyo ni kuhakikisha miradi itakayobuniwa inakuwa na manufaa ya moja kwa moja kwa wananchi na kuchochea kasi ya maendeleo katika maeneo mbalimbali ya kata hiyo.

Aidha, katika mazungumzo hayo, viongozi hao wamejadili pia mwenendo wa mvua na namna ya kuhakikisha wananchi wanakuwa salama katika kipindi hiki cha mvua.

Kwa upande wake, katibu tawala wa wilaya Asha Churu amesisitiza umuhimu wa wananchi kuendelea kufuatilia taarifa sahihi za utabiri wa hali ya hewa zinazotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), pamoja na kuzingatia tahadhari na maelekezo yanayotolewa kabla, wakati na baada ya mvua ili kujikinga na madhara yanayoweza kujitokeza.

Ushirikiano kati ya viongozi na taasisi za Serikali ni muhimu katika kuimarisha utoaji wa huduma, kubuni fursa za kiuchumi na kuharakisha maendeleo yanayomgusa mwananchi moja kwa moja.
logoblog
Previous
« Prev Post