.
Na Suzy Butondo,Tabora
Diwani wa Kata ya Chemchem, Manispaa ya Tabora, Bandora Salum Mirambo, amefanya mkutano wa hadhara na wananchi wa kata hiyo kwa lengo la kusikiliza kero zinazowakabili na kujadili mikakati ya kuboresha maendeleo ya kata miundombinu, usafi wa mazingira pamoja na kuchukua tahadhari dhidi ya mvua za El Niño.

Mkutano huo uliwakutanisha maafisa kutoka Ofisi ya Mkurugenzi, watendaji na maafisa wa kata, wenyeviti wa mitaa pamoja na wananchi ambao walipata fursa ya kueleza changamoto zinazowakabili katika maeneo yao na kutoa maoni kuhusu namna ya kuzitatua.
Akizungumza katika mkutano huo, Diwani Bandora aliwataka wananchi kuendelea kuchukua tahadhari za mapema ili kupunguza athari zinazoweza kusababishwa na mvua za El Niño.
Alisisitiza umuhimu wa kufanya usafi wa mazingira, kufukua mitaro iliyoziba, kuondoa taka zinazozuia upitishaji wa maji na kufuatilia taarifa za utabiri wa hali ya hewa ili kujiandaa kukabiliana na changamoto zinazoweza kujitokeza wakati wa mvua.
WANANCHI WAELEZA KERO ZA MIUNDOMBINU NA SHULE
Kwa upande wao, wananchi walitumia mkutano huo kueleza changamoto mbalimbali zinazowakabili, zikiwemo ubovu wa miundombinu ya barabara pamoja na kujaa kwa maji katika maeneo ya Shule ya Msingi Chemchem.
Wananchi hao wameeleza kuwa hali ya maji kujaa katika eneo la shule hiyo huwasababishia wanafunzi adha wanapokwenda na kurudi shuleni, hususan katika kipindi cha masika.
Aidha, walieleza changamoto ya kuchakaa kwa majengo ya shule na kutokamilika kwa ujenzi wa madarasa, hali inayohitaji hatua za pamoja ili kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia.
Changamoto hizo zimeibua umuhimu wa kuimarisha miundombinu ya barabara na mifereji ya maji, pamoja na kufuatilia mahitaji ya shule ili kuhakikisha wanafunzi wanapata mazingira bora na salama ya kujifunzia.
BANDORA AHAIDI KUFUATILIA KERO ZA WANANCHI
Akijibu hoja zilizowasilishwa na wananchi, Diwani Bandora amesema amezipokea changamoto zote zilizotolewa na kwamba zitafuatiliwa kwa kushirikiana na mamlaka na wataalamu husika ili kutafuta ufumbuzi.
Amesema baadhi ya changamoto zimeanza kushughulikiwa, huku akiahidi kuendelea kufanya vikao vya mara kwa mara na wananchi ili kupata maoni yao, kusikiliza kero zinazowakabili na kujadili hatua za kuboresha huduma na maendeleo ya kata hiyo.
Amesisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya wananchi, viongozi wa mitaa, serikali na wataalamu katika kutatua changamoto zinazojitokeza na kuhakikisha shughuli za maendeleo zinatekelezwa kwa manufaa ya jamii.
Mkutano huo pia umejadili masuala mbalimbali yanayohusu maendeleo ya Kata ya Chemchem, uboreshaji wa miundombinu, usafi wa mazingira na kuimarisha ushirikiano kati ya wananchi na serikali katika kutatua changamoto za kijamii.
Kupitia mikutano ya aina hiyo, wananchi wanapata fursa ya kuwasilisha maoni na kero zao moja kwa moja kwa viongozi, huku viongozi wakipata nafasi ya kufahamu mahitaji ya wananchi na kujadili hatua zinazoweza kuchukuliwa kwa ajili ya maendeleo ya kata.