
Tabora
Mwenyekiti wa Kamati ya Mipango Miji, Ujenzi na Mazingira ya Manispaa ya Tabora, ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Chemchem, Bandora Salum Mirambo, amewataka wananchi kujenga utamaduni wa kufanya usafi katika maeneo yao kwa hiari, badala ya kusubiri kushurutishwa na viongozi.
Bandora amekuwa akitembelea baadhi ya kata na kutoa elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa usafi wa mazingira. Amesisitiza kuwa usafi unapaswa kuwa sehemu ya maisha ya kila siku ya kila mwananchi, ikiwemo kusafisha maeneo yanayowazunguka na kutupa taka katika maeneo maalumu yaliyotengwa na serikali za mitaa.
Amesema usafi wa mazingira ni wajibu wa kila mwananchi, hivyo wananchi wanapaswa kushiriki kikamilifu katika kuhakikisha maeneo yao ya makazi, biashara na maeneo ya umma yanakuwa safi na salama.
Bandora ameahidi kuendelea kutoa elimu kwa wananchi pamoja na kusimamia utekelezaji wa shughuli za usafi katika maeneo mbalimbali, kwa lengo la kuifanya Manispaa ya Tabora kuwa safi, salama na yenye mazingira bora.
Aidha, amesema kufanya usafi ni jukumu la kisheria na kijamii linalolenga kulinda afya za wananchi, kupunguza hatari ya magonjwa ya mlipuko na kuhakikisha mazingira ya makazi na biashara yanatunzwa ipasavyo.


