
Na Suzy Butondo, Shinyanga
Naibu Meya wa Manispaa ya Shinyanga, Pendo Sawa, amewaagiza Maafisa Maendeleo ya Jamii ngazi ya kata kuacha utaratibu wa kusubiri wananchi ofisini na badala yake kuwafuata katika maeneo yao kwa lengo la kuwapatia elimu itakayowawezesha kunufaika na mikopo inayotolewa na halmashauri.
Pendo alitoa maelekezo hayo leo, Julai 25, 2026, wakati akizungumza na wanachama wa Umoja wa Wanawake wa Chama Cha Mapinduzi (UWT) kutoka kata za Masekelo na Lubaga, kwenye ziara ya kamati ya utekelezaji ya UWT wilaya ya Shinyanga mjini
Alisema maafisa hao wanapaswa kutoa elimu kuhusu taratibu sahihi za usajili wa vikundi, uandaaji wa katiba na uandishi wa maandiko ya miradi ili vikundi viweze kukidhi vigezo vya kupata mikopo ya halmashauri.
Alibainisha kuwa wananchi wengi, hususan wanawake, vijana na watu wenye ulemavu, wamekuwa wakikosa fursa ya kunufaika na mikopo hiyo kutokana na ukosefu wa elimu sahihi kuhusu masharti na taratibu za uombaji, hali inayochangia kuendelea kwa malalamiko kutoka kwa walengwa.
Kwa mujibu wa Mhe. Pendo, utoaji wa elimu kwa wananchi utaongeza idadi ya vikundi vinavyokidhi vigezo vya kupata mikopo na kuhakikisha fedha zinazotengwa na halmashauri zinawanufaisha walengwa waliokusudiwa kwa lengo la kuinua uchumi wao.
Aidha, aliwataka Maafisa Mifugo ngazi ya kata kuimarisha utoaji wa elimu kuhusu ufugaji bora ili wafugaji waweze kuongeza tija, kuboresha uzalishaji na kutumia kikamilifu fursa za kiuchumi zinazotokana na sekta ya mifugo.
Alisisitiza kuwa watumishi wa halmashauri wanapaswa kuwa karibu na wananchi kwa kuwafikia moja kwa moja badala ya kusubiri huduma zitafutwe ofisini, ili kuhakikisha jamii inanufaika na fursa zote za maendeleo zinazotolewa na Serikali.
Ziara hiyo ya UWT Wilaya ya Shinyanga Mjini inaongozwa na Mwenyekiti wa UWT wilayani humo, Rehema Nhamanilo. Leo, Julai 25, 2026, viongozi hao walitembelea kata za Mwawaza, Masekelo na Lubaga, ambako walikutana na wanachama pamoja na wananchi, wakasikiliza na kupokea kero mbalimbali zilizowasilishwa na wanawake.
Kero hizo zilipatiwa ufafanuzi na majibu na viongozi pamoja na wataalamu waliokuwapo. Sambamba na hilo, zoezi la ulipaji wa ada za wanachama na uandikishaji wa wanachama wapya lilifanyika kwa lengo la kuendelea kuimarisha chama.