
Diwani wa Kata ya Chemchem, Bandora Salumu Mirambo.
Na Suzy Butondo, Shinyanga
Diwani wa Kata ya Chemchem, Bandora Salumu Mirambo, amewatakia Watanzania wote, hususan wananchi wa Kata ya Chemchem, Kheri ya Kumbukumbu ya Siku ya Mashujaa, huku akiwahimiza kuenzi mchango wa mashujaa wa taifa kwa vitendo kupitia kudumisha amani, umoja na mshikamano.
Akitoa salamu zake katika maadhimisho ya siku hiyo ya kitaifa, Diwani Bandora amesema Siku ya Mashujaa ni fursa muhimu ya kuwakumbuka na kuwaenzi wazalendo waliotoa maisha, nguvu na muda wao kwa ajili ya kupigania na kulinda uhuru, amani, usalama na umoja wa Tanzania.
Amesema maadhimisho hayo yanapaswa kuwa chachu ya kuimarisha uzalendo na kuwakumbusha Watanzania wajibu wao wa kushiriki katika maendeleo ya taifa, huku wakidumisha amani ambayo imeendelea kuwa msingi wa mafanikio ya nchi.
"Tuwakumbuke mashujaa wetu kwa vitendo kwa kudumisha amani, umoja na mshikamano wa Taifa letu. Tujenge Tanzania yenye maendeleo kwa kizazi cha sasa na kijacho," amesema Bandora
Aidha, amewaomba wananchi kuendelea kushirikiana katika kujenga jamii yenye mshikamano, kuheshimiana na kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo ili kuenzi kwa vitendo mchango wa mashujaa walioijenga Tanzania.
Mungu Ibariki Kata ya Chemchem.
Mungu Ibariki Tanzania. 🇹🇿