KAMPENI YA MSAADA WA KISHERIA KUANZA SHINYANGA, WANANCHI WAHIMIZWA KUJITOKEZA | BUTONDO DIGITAL

Tuesday, May 5, 2026

KAMPENI YA MSAADA WA KISHERIA KUANZA SHINYANGA, WANANCHI WAHIMIZWA KUJITOKEZA

  Suzy Butondo       Tuesday, May 5, 2026
Mkuu wa mkoa wa Shinyanga Mboni Mhita akizungumza

Na Suzy Butondo, Shinyanga

Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mboni Mhita, amewahimiza wananchi wa mkoa wa Shinyanga  kujitokeza kwa wingi kushiriki kampeni ya kitaifa ya Samia Legal Aid   inayolenga kutoa huduma mbalimbali za kisheria pamoja na kutatua migogoro ya kijamii.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Mei 5, 2026, ofisini kwake, Mhita amesema kampeni hiyo itafanyika kuanzia Mei 6 hadi Mei 20, 2026, ikiwa ni sehemu ya jitihada za Serikali ya Awamu ya Sita kuhakikisha wananchi wanapata haki na huduma za kisheria kwa urahisi zaidi.

Amesema lengo kuu la kampeni hiyo ni kuimarisha upatikanaji wa haki kwa makundi mbalimbali ya kijamii, yakiwemo wanawake, vijana, watu wenye ulemavu na wazee.

Mhita ameeleza kuwa tayari timu ya watoa huduma za msaada wa kisheria imejipanga kufika katika kata zote 130 za mkoa huo ili kuwafikia wananchi wengi zaidi na kutoa elimu pamoja na ushauri wa kisheria.

"Serikali ya mama yetu mama Samia imejitolea kuwasaidia wananchi msaada wa kisheria bure kabisa, hivyo niwaombe wananchi wote mjitokeze kuanzia kesho tarehe sita kuja kupatiwa huduma mbalimba za kisheria na kupata uelewa mpana wa kisheria, mama Samia ametukumbuka tena tuchangamkie fursa hii"amesema Mhita 


Ameongeza kuwa hii ni awamu ya pili ya kampeni hiyo katika mkoa wa Shinyanga, ambapo awamu ya kwanza iliyofanyika Aprili 2023 ilishughulikia jumla ya migogoro 578, kati ya hiyo migogoro 378 ilitatuliwa, huku zaidi ya wananchi 22,000 wakinufaika na huduma hizo. 

Aidha Mhita ameyataja maeneo ya kutolea huduma hizo za kisheria, katika manispaa ya Shinyanga itafanyika maeneo ya Nguzo nane zimamoto, halmashauri ya Kishapu watafanyia eneo la Mhunze maeneo ya mnadani na kata  ya ukenyenge,  wilaya ya Shinyanga watakuwa Didia na Iselamagazi, manispaa ya Kahama watafanyia  maeneo ya  Shunu karibu na ofisi ya mtendaji na Majengo, Msalala watafanyia Isaka uwanja wa Isaka na Segese , Ushetu watafanyia kata ya Bulungwa na Nyamilangano senta. 


Kwa upande wake, Mkurugenzi Msaidizi wa Uzingatiwaji wa Msaada wa Kisheria, Osborn Paiss, amesema kampeni hiyo itatekelezwa kwa siku 15 na itahusisha wataalamu mbalimbali wakiwemo wanasheria, wataalamu wa ardhi pamoja na maafisa wa dawati la polisi.

Amesema timu hizo zitawafikia wananchi katika maeneo mbalimbali ikiwemo mashuleni, masokoni na kupitia mikutano ya hadhara, kwa lengo la kutoa elimu ya kisheria na kusaidia kupunguza migogoro, hususan ya ardhi na mipaka.

Aidha, Paiss ameeleza kuwa kampeni ya mwaka huu itajumuisha huduma za ushauri wa kisheria, elimu kwa umma, uandaaji wa nyaraka za kisheria pamoja na uwakilishi katika vyombo vya mahakama.

Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Kisheria Mkoa wa Shinyanga, John Shija, amesema wanatarajia mafanikio makubwa katika awamu hii ya pili, huku akiwahimiza wananchi kujitokeza kwa wingi kunufaika na huduma hiyo ya bure.













logoblog
Newest
You are reading the newest post