JUMUIYA YA WAZAZI KATA YA NGOKOLO YATOA MSAADA KWA WAGONJWA KITUO CHA AFYA NGOKOLO | BUTONDO DIGITAL

Friday, May 8, 2026

JUMUIYA YA WAZAZI KATA YA NGOKOLO YATOA MSAADA KWA WAGONJWA KITUO CHA AFYA NGOKOLO

  Suzy Butondo       Friday, May 8, 2026

Na Suzy Butondo, Shinyanga

Jumuiya ya Wazazi Wilaya ya Shinyanga Mjini imewaomba viongozi wa dini, wazazi na walezi kuendelea kukemea vitendo viovu vinavyofanywa na watoto na vijana ili waweze kurejea katika maadili mema ya kimungu na kitanzania.

Wito huo umetolewa na mjumbe wa Kamati ya Utekelezaji ya Jumuiya ya Wazazi Wilaya ya Shinyanga Mjini, Giti Boniphace, wakati wa maadhimisho ya Wiki ya Wazazi yaliyofanyika katika Kata ya Ngokolo. Katika maadhimisho hayo, jumuiya hiyo ilitoa zawadi mbalimbali kwa wagonjwa waliolazwa katika Kituo cha Afya Ngokolo.

Akizungumza katika hafla hiyo, Boniphace aliwataka viongozi wa dini kuhakikisha wanatumia majukwaa yao kufundisha maadili na kukemea maovu yanayofanywa na watoto na vijana.

“Naomba makanisa na misikiti tukemee vitendo vibaya vinavyofanywa na watoto wetu. Wazazi wengi wamekuwa wakikata tamaa na kusema watoto watajijua wenyewe. Tusikate tamaa, turudi kwenye malezi bora na tuwaonye wanapokosea,” amesema Boniphace.

Aidha, amesisitiza umuhimu wa wazazi kuwahamasisha watoto kusoma kwa bidii na kushirikiana na walimu katika malezi yao badala ya kuwachukia wanapochukua hatua za kinidhamu.

“Mimi nisingefika hapa nilipo kama wazazi wangu wangeniacha niharibike. Walinisimamia imara. Tuwahimize watoto wetu kusoma na tushirikiane na walimu katika kuwalea,” ameongeza.

Kwa upande wake, mjumbe wa Baraza la Wazazi Wilaya ya Shinyanga Mjini, Hasna Maige, amesema jukumu la mzazi ni kuhakikisha watoto wanalelewa katika maadili bora huku wakikingwa dhidi ya ukatili na mazingira hatarishi.

Naye Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi Kata ya Ngokolo, Khamis Genda Mabula, amesema maadhimisho ya Wiki ya Wazazi kwa mwaka huu yamelenga kuonesha upendo kwa jamii kupitia utoaji wa zawadi kwa wagonjwa katika Kituo cha Afya Ngokolo ili kuwafariji na kuwapa faraja.


Kwa upande mwingine, mjumbe wa Jumuiya ya Wazazi Tawi la Ngokolo ambaye pia ni mjumbe wa Msalizano Wilaya ya Shinyanga Mjini, Masoud Mlowe, amesema kwa sasa kuna ongezeko la mmomonyoko wa maadili kwa vijana, hivyo wazazi wanapaswa kushirikiana kwa karibu na walimu katika kurekebisha tabia za watoto wao.

“Watoto wanapokosea shuleni, wazazi wasiingie kwa hasira kwa walimu. Waende kwa utulivu kujua makosa na namna ya kuyarekebisha. Malezi bora yanaendana na mafundisho ya dini,” amesema Mlowe.

Mwenyekiti wa UWT Kata ya Ngokolo, Hulda Massaba amesema wamepokea maelekezo yaliyotolewa na viongozi hao na kuahidi kuyafanyia kazi kwa vitendo.

“Ni kweli wakati mwingine sisi wenyewe tunaruhusu watoto kwenda kuzurura hovyo. Tunashukuru kwa kutukumbusha umuhimu wa kuwalea watoto wetu katika maadili mema,” amesema Massaba.

Dkt. Baraka Sule, ambaye ni mmoja wa waganga wa kituo hicho, ameshukuru kwa zawadi hizo na kuiomba jumuiya ya wazazi, inapopata nafasi, iendelee kuwatembelea kwani wagonjwa wamefarijika sana kwa kupata zawadi hizo





























































































logoblog
Newest
You are reading the newest post