.jpg)
Kamanda wa jeshi la polisi mkoa wa Shinyanga Janeth Magomi akizungumza na waandishi wa habari
Na Suzy Butondo, Shinyanga,
BUTONDO DIGITAL
Watu wawili, Kisaka Elinihaki (22), mfanyabiashara, na Makoye James (20), dereva, wote wakazi wa Manispaa ya Kahama, wamehukumiwa vifungo vya jela kwa kosa la kutoa taarifa za uongo.
Kamanda wa jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga, Janeth Magomi, akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake leo Aprili 9, 2026, amesema kuwa Aprili 7, 2026 jeshi hilo liliwakamata watuhumiwa hao kwa tuhuma hizo.
Amesema watuhumiwa walidai kuwa sehemu zao za siri zimepotea kimiujiza baada ya kuguswa bega, jambo lililosababisha taharuki kubwa katika jamii.
Kwa mujibu wa Kamanda Magomi, watuhumiwa hao walifikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Kahama, ambapo walipatikana na hatia ya kutoa taarifa za uongo zilizosababisha taharuki.
Katika hukumu hiyo, Kisaka Elinihaki alihukumiwa kifungo cha miezi sita jela, huku Makoye James akihukumiwa kifungo cha miezi mitano jela.
Aidha, Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga limewakumbusha wananchi kuwa kutoa taarifa za uongo ni kosa la jinai linaloweza kusababisha taharuki katika jamii. Polisi wameendelea kusisitiza umuhimu wa kutoa taarifa sahihi na kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama ili kudumisha amani na utulivu.
“Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga tumejipanga vyema kukabiliana na uhalifu wa aina yoyote, ikiwemo uhamiaji haramu. Kwa sasa hali ni shwari na tunaendelea kudhibiti uhalifu,” amesema Kamanda Magomi.