Katibu Tawala Mkoa wa Shinyanga, CP. Salum Hamduni, amewataka wazazi na walezi kuhakikisha watoto wote wanapatiwa chanjo ya Polio ili kuwakinga dhidi ya ugonjwa huo unaoweza kusababisha ulemavu wa kudumu au kifo.
Akizungumza leo Machi 23, 2026 katika kikao kazi cha hamasa ya kampeni ya chanjo ya Polio mkoani humo, Hamduni amesema kampeni hiyo itafanyika kuanzia Machi 24 hadi 27, 2026, ikilenga kuwafikia watoto 781,166 wenye umri chini ya miaka 10.
Kwa upande wake, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Dkt.Yudas Ndungile, amesema Serikali imeanzisha kampeni hiyo kufuatia kubainika kwa vimelea vya Polio katika maji taka jijini Mwanza, hali inayoongeza hatari ya maambukizi.
“Polio haina tiba, lakini inazuilika kwa chanjo. Ni muhimu wazazi kuhakikisha watoto wao wanapata chanjo hii kwa wakati,” amesema Dkt. Ndungile.
Amesisitiza kuwa chanjo hiyo ni salama kwa watoto wote walio chini ya miaka 10, na kuonya kuwa mtoto atakayekosa chanjo atakuwa kwenye hatari kubwa ya kupata ugonjwa huo.
Naye Mratibu wa Miradi ya Afya ya Uzazi na Mtoto kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI, Dinah Atinda, amesema ana imani kuwa Mkoa wa Shinyanga utafanikiwa kufikia malengo ya kampeni hiyo kutokana na maandalizi yaliyofanyika.
Kwa upande wake, mwakilishi kutoka Wizara ya Afya, Anne Shima, amesema vifaa tiba vimesambazwa katika halmashauri zote na jumla ya wahudumu wa afya 1,486 wameandaliwa kuhakikisha huduma hiyo inatolewa kwa ufanisi.
Baadhi ya washiriki wa kikao hicho wameipongeza Serikali kwa jitihada za kulinda afya ya watoto, wakieleza kuwa uwekezaji katika afya ya mtoto ni msingi wa kulinda kizazi cha baadaye na maendeleo ya taifa.
Wazazi Watakiwa Kuwapeleka Watoto Chanjo ya Polio Kuepuka Ulemavu”






