Tabora
Rhino Rangers imeanza vyema safari yake ya Championship League msimu wa 2026/2027, baada ya kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Tanzania Prisons katika mchezo uliopigwa kwenye Uwanja wa Ally Hassan Mwinyi, Tabora.
Ushindi huo umeupa nguvu mpya upande wa Rhino Rangers katika harakati za kurejea kwenye Ligi Kuu ya Tanzania, huku timu hiyo ikianza safari hiyo kwa hatua nzuri.
Makamu Mwenyekiti wa Rhino Rangers, Bandora Salum Mirambo, amewapongeza wachezaji kwa kuonesha kiwango kizuri na kupambana hadi kupata ushindi katika mchezo huo.
Bandora amesema ushindi huo ni mwanzo mzuri wa safari ya timu kuelekea Ligi Kuu, huku akiwapongeza pia mashabiki wa Rhino Rangers, maarufu kama “Wanafaru,” kwa kujitokeza kwa wingi kuishangilia timu yao.
Amesema uwepo na sapoti ya mashabiki ni sehemu muhimu ya mafanikio ya timu, hivyo amewataka mashabiki, wadau na wananchi kwa ujumla kuendelea kuiunga mkono Rhino Rangers katika michezo ijayo.
“Tumeanza safari ya kurejea Ligi Kuu kwa ushindi. Kituo kinachofuata ni Songea,” amesema Bandora.
Rhino Rangers sasa inaelekeza nguvu zake kwenye mchezo unaofuata huko Songea, ikiwa na matumaini ya kuendeleza kasi nzuri iliyoianza katika mchezo wa kwanza.
.jpg)