Mwenyekiti wa Kamati ya Mipango Miji, Ujenzi na Mazingira, Salum Bandora, amewatia moyo wananchi wa Inala, Kata ya Ndevelwa, kwa kuwapongeza kwa juhudi zao katika ujenzi wa Ofisi ya Kijiji cha Inala.
Bandola ametoa pongezi hizo wakati wa ziara ya kukagua maendeleo ya miradi ya ujenzi katika eneo hilo, akieleza kuridhishwa na kazi kubwa inayofanywa na wananchi pamoja na jitihada zao za kuhakikisha ujenzi wa ofisi hiyo unakamilika.
Katika kuunga mkono juhudi za wananchi hao, Bandora alichangia mifuko mitano ya saruji kwa ajili ya kuendeleza ujenzi wa Ofisi ya Kijiji cha Inala.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Bandora aliwataka wananchi kuendelea kushirikiana na kudumisha moyo wa kujitolea katika kutekeleza miradi ya maendeleo inayolenga kuboresha huduma na mazingira ya maisha katika maeneo yao.
“Nawatia moyo wananchi wa Inala, Kata ya Ndevelwa, kwa kazi kubwa mliyoifanya na mnayoendelea kuifanya. Nimeamua kuchangia mifuko mitano ya saruji ili kuunga mkono juhudi zenu,” amesema Bandora.
Mbali na kukagua ujenzi wa Ofisi ya Kijiji cha Inala, Kamati hiyo pia ilikagua ujenzi wa Jengo la Mama na Mtoto Manoleo pamoja na Ofisi ya Mtendaji wa Kata ya Misha.
Ukaguzi huo ni sehemu ya juhudi za kufuatilia maendeleo ya miradi ya ujenzi na kuhakikisha inatekelezwa kwa kuzingatia viwango vinavyotakiwa, kwa lengo la kuwawezesha wananchi kupata huduma bora.
Bandora amesisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya wananchi na viongozi katika kusimamia na kukamilisha miradi ya maendeleo kwa wakati.





