Wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, Rais aliahidi kuifufua Kigoma na kuirejeshea hadhi yake kama kitovu muhimu cha uchumi, biashara na usafiri katika ukanda wa Magharibi mwa Tanzania. Ahadi hiyo inaendelea kutekelezwa kwa vitendo kupitia uwekezaji mkubwa katika miundombinu ya usafiri na uchukuzi.
Katika hatua nyingine ya utekelezaji wa ahadi hiyo, Rais amezindua ujenzi wa meli nne za mizigo, ameweka jiwe la msingi la ujenzi wa reli ya kisasa (SGR) kwa kipande cha sita kutoka Tabora hadi Kigoma, na kukagua maendeleo ya ujenzi wa gati jipya la abiria pamoja na uboreshaji wa gati la mizigo katika Bandari ya Kigoma.
Miradi hiyo ni sehemu ya mkakati mpana wa Serikali wa kuimarisha sekta ya usafiri na uchukuzi kwa kujenga mtandao wa kisasa unaounganisha maeneo ya uzalishaji na masoko ya ndani na nje ya nchi. Kupitia uwekezaji unaoendelea katika bandari, reli, viwanja vya ndege na barabara, Tanzania inaendelea kujiimarisha kama kitovu cha biashara na uwekezaji katika Afrika Mashariki na Kati.
Mbali na kuboresha huduma za usafiri na usafirishaji wa mizigo, miradi hiyo inatarajiwa kupunguza gharama za usafirishaji, kuongeza ufanisi wa biashara, kuvutia uwekezaji zaidi na kufungua maelfu ya fursa za ajira kwa wananchi.
Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Rais alisisitiza kuwa mafanikio ya miradi hiyo yatategemea ushirikiano wa wananchi na Serikali. Aliwataka Watanzania kuendelea kudumisha amani, umoja na utulivu, akieleza kuwa hayo ndiyo msingi wa maendeleo endelevu.
Aidha, aliwahimiza wananchi kujitayarisha kutumia kikamilifu fursa za kiuchumi zitakazotokana na miradi hiyo ili kuongeza kipato cha mtu mmoja mmoja na kuchochea ukuaji wa uchumi wa taifa.
Rais pia alitoa wito kwa wananchi kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama katika kulinda miundombinu hiyo, akisisitiza kuwa hujuma yoyote dhidi ya miradi ya maendeleo ni hasara kwa taifa zima.
Utekelezaji wa miradi hii unaendelea kuonesha dhamira ya Serikali ya kuboresha miundombinu ya kimkakati, kuunganisha Tanzania na masoko ya kikanda na kimataifa, na kuhakikisha uwekezaji katika sekta ya usafiri unakuwa chachu ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwa vizazi vya sasa na vijavyo.



